13 “ ‘Maana mfalme wa kaskazini baadaye ataandaa jeshi kubwa kuliko lile la awali. Kisha baada ya miaka kadhaa atarudi na jeshi kubwa lenye vifaa vingi.
14 Wakati huo watu wengi watamwasi mfalme wa kusini. Baadhi ya watu wakatili wa taifa lako Danieli, wataasi ili kutekeleza maono haya, lakini hawatafaulu.
15 Ndipo mfalme wa kaskazini atauzingira mji wenye ngome imara na kuuteka. Wanajeshi wa kusini hawatastahimili, hata wale wateule, maana hawatakuwa na nguvu.
16 Mvamizi atawatenda kama apendavyo, hakuna atakeyethubutu kupingana naye. Atasimama katika nchi tukufu, na nchi hiyo yote itakuwa chini ya mamlaka yake.
17 “ ‘Huyo mvamizi atakusudia kuja na jeshi lake lote, naye atafanya mapatano na kuyatekeleza. Atamwoza binti mmoja ili kuuangamiza ufalme wa adui yake; lakini mpango wake hautafaulu, wala kumfaidia lolote.
18 Baadaye, atazigeukia na kuzishambulia nchi nyingi za pwani na kuzishinda. Lakini jemadari mgeni atamshinda na kuyakomesha majivuno yake mwenyewe; naam, atamrudishia mfalme wa kaskazini majivuno yake mwenyewe.
19 Hapo atageuka kurudi katika ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka vitani na huo ndio utakaokuwa mwisho wake.