21 Basi, vijana hao wakafungwa hali wamevaa makoti yao, kanzu zao, kofia na mavazi yao mengine, wakatupwa katikati ya ile tanuri ya moto mkali.
22 Kwa vile amri ya mfalme ilikuwa kali, ule moto ulikuwa umewashwa ukawa mkali sana, hata ndimi za moto zikawateketeza wale watu waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego.
23 Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego, wakiwa wamefungwa, wakatumbukia katika ile tanuri ya moto mkali.
24 Basi, mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hatukuwafunga watu watatu na kuwatupa motoni?” Nao wakamjibu mfalme, “Naam, mfalme! Ndivyo!”
25 Kisha akauliza, “Lakini sasa mbona ninaona watu wanne wakitembeatembea humo motoni bila kufungwa na wala hawadhuriki, na mtu wa nne anaonekana kama mwana wa miungu?”
26 Basi, mfalme Nebukadneza akaukaribia mlango wa tanuri ya moto mkali, akaita, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Mkuu, tokeni mje hapa!” Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka motoni.
27 Maliwali, wasimamizi, wakuu wa mikoa na washauri wa mfalme, wote wakakusanyika pamoja, wakaona ya kuwa ule moto haukuweza kuwaunguza hao watatu. Nywele zao hazikuungua, mavazi yao hayakuungua, wala hawakuwa na harufu yoyote ya moto.