10 Haya yote yatatendeka ili waweze kumtolea Mungu wa mbinguni tambiko zinazompendeza na waombee maisha yangu mimi mfalme na watoto wangu.
11 Naamuru pia kwamba mtu yeyote ambaye hatatii amri hii, boriti ingolewe kutoka katika nyumba yake, na atumbuliwe kwayo. Tena, nyumba yake na ifanywe kuwa rundo la mavi.
12 Mungu aliyeuchagua mji wa Yerusalemu kuwa mahali pake pa kuabudiwa na amwangushe mfalme au taifa lolote litakalopinga amri hii au kutaka kuiharibu nyumba hii ya Mungu iliyoko mjini Yerusalemu. Mimi Dario nimetoa amri hii. Ni lazima ifuatwe.’”
13 Basi, Tatenai, mtawala wa mkoa wa magharibi ya mto Eufrate, Shethar-bozenai, na maofisa wenzao, wakafanya bidii kutekeleza maagizo ya mfalme.
14 Viongozi wa Wayahudi waliendelea vizuri sana na kazi ya ujenzi wa hekalu, wakitiwa moyo kwa mahubiri ya nabii Hagai na Zekaria, mwana wa Ido. Walimaliza ujenzi wa hekalu kama walivyoamriwa na Mungu wa Israeli, na kama walivyoagizwa na mfalme Koreshi, mfalme Dario na mfalme Artashasta, wa Persia.
15 Ujenzi wa nyumba hiyo ulimalizika mnamo siku ya tatu ya mwezi wa Adari, katika mwaka wa sita wa utawala wa mfalme Dario.
16 Basi, watu wa Israeli, makuhani, Walawi na watu wengine waliokuwa wamerudi kutoka uhamishoni waliiweka wakfu nyumba ya Mwenyezi-Mungu kwa shangwe kuu.