4 Mfuateni na kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kushika amri zake na kuitii sauti yake; mtumikieni na kuambatana naye.
5 Lakini nabii huyo au mtabiri wa ndoto atauawa, kwa sababu atakuwa amewafundisha uasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka utumwani, ili muiache njia ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwaamuru muifuatea. Hivyo ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
6 “Ikiwa ndugu yako wa tumbo moja, au mtoto wako wa kiume au wa kike, au mke wako umpendaye sana, au rafiki yako mwandani, atakushawishi kwa siri akisema, ‘Twende tukaabudu miungu mingine’, miungu ambayo wewe wala babu zenu hamuijui,
7 au baadhi ya miungu ya watu wanaoishi karibu nanyi, au miungu ya watu waishio mbali toka ncha moja ya dunia hadi nyingine,
8 usikubali kushawishiwa, wala usimsikilize au kumhurumia, wala usimwachilie wala kumficha;
9 bali utamuua. Wewe utakuwa wa kwanza kuchukua hatua ya kumuua, kisha watu wengine wote watafuata.
10 Mpigeni mawe mpaka afe! Kwa sababu amejaribu kukuvutia mbali na Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, aliyekutoa utumwani nchini Misri.