12 Naye mtu asiyejali kumtii kuhani au mwamuzi aliyewekwa hapo kumhudumia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au mwamuzi, mtu huyo atauawa. Ndivyo mtakavyokomesha uovu miongoni mwenu.
13 Watu wote watasikia na kuogopa wasifanye tena kitu kwa kutojali.
14 “Mtakapokwisha ingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni, mkaimiliki na kukaa humo, nanyi mkasema, ‘Tutaweka mfalme juu yetu, kama mataifa yote yanayotuzunguka;’
15 mwaweza kumweka mfalme juu yenu mtu ambaye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atamchagua. Mtamweka mmojawapo wa ndugu zenu kuwa mfalme juu yenu. Msimfanye mgeni asiye ndugu yenu kuwa mfalme wenu.
16 Hata hivyo, asiwe na farasi wengi kwa ajili yake mwenyewe, wala asiwarudishe watu Misri ili kujipatia farasi zaidi, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amewaonya, ‘Kamwe msirudi huko tena’.
17 Wala asijipatie wake wengi, la sivyo moyo wake utaasi; wala asijipatie fedha na dhahabu kwa wingi mno.
18 Atakapokuwa amekalia kiti cha ufalme lazima afanye nakala ya sheria hii iandikwe mbele ya makuhani wa Kilawi.