7 Kwa hiyo mimi nawaamuru mtenge miji mitatu.
8 “Tena kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ataipanua mipaka ya nchi yenu, kama alivyowaapia babu zenu, naye akawapatia nchi yote ambayo aliahidi kuwapatia hao babu zenu
9 ikiwa mtakuwa waangalifu kushika amri hizi zote ninazowaamuru hivi leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata siku zote njia zake – basi, mtaongeza miji mingine mitatu zaidi ya hii mitatu,
10 ili mtu asiye na hatia asije akauawa katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapatia kuwa yenu, na hivyo kuwasababisha kuwa na hatia ya mauaji.
11 “Lakini mtu akiwa adui wa mwenzake, akamvizia akamshambulia na kumuua, kisha akakimbilia kwenye mji mmojawapo wa miji hiyo,
12 hapo wazee wa mji huo watatuma watu wamtoe huko na kumkabidhi kwa mwenye kulipiza kisasi cha umwagaji damu, auawe.
13 Msimwonee huruma, bali mtaukomesha uovu wa mauaji ya mtu asiye na hatia katika Israeli, ili mpate kuishi kwa amani.