1 “Mkienda vitani kupigana na adui zenu, mkaona farasi, magari na jeshi kubwa zaidi kuliko lenu msiwaogope. Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliyewatoa Misri, atakuwa nanyi.
2 Kabla ya kuanza mapigano, kuhani atajitokeza mbele na kuwaambia watu,
3 ‘Watu wa Israeli sikilizeni! Leo mnakaribia kupigana dhidi ya adui zenu. Msife moyo, au kuogopa, au kutishika, au kuwaogopa adui;
4 maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye atakayekwenda pamoja nanyi kupigana kwa niaba yenu dhidi ya adui zenu na kuwapa ushindi.’
5 “Kisha maofisa watawaambia watu: ‘Kuna mtu yeyote hapa aliyejenga nyumba mpya lakini hajaizindua? Arudi nyumbani, asije akafia vitani na mtu mwingine akaizindua.
6 Kuna mtu yeyote hapa aliyepanda mizabibu na ambaye hajafurahia matunda yake ya kwanza? Arudi nyumbani asije akafia vitani na mtu mwingine akafurahia matunda yake.
7 Kuna mwanamume yeyote hapa aliyeposa na yuko karibu kuoa? Arudi nyumbani, asije akafia vitani, na mwanamume mwingine akaoa mchumba wake.’