3 Utafanya vivyo hivyo kuhusu punda au vazi au kitu chochote ambacho nduguyo amekipoteza. Kamwe usiache kumsaidia.
4 “Ukiona punda au ng'ombe wa nduguyo ameanguka njiani, usiache kumsaidia nduguyo; utamsaidia kumwinua.
5 “Wanawake wasivae nguo za wanaume, na wanaume wasivae nguo za wanawake. Anayefanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
6 “Ukikuta kiota cha ndege mtini au njiani, kina makinda au mayai na mamandege ameyafunika hayo makinda au mayai, usimchukue mamandege na makinda yake.
7 Utamwacha mamandege aende zake, lakini unaweza kuchukua makinda. Ukifanya hivyo utafanikiwa na kuishi maisha marefu.
8 “Unapojenga nyumba, jenga ukingo pembeni mwa paa, usije ukalaumiwa kama mtu akianguka kutoka huko, akafa.
9 “Usipande mizabibu yako pamoja na mimea mingine, la sivyo mazao yote yatakuwa haramu, siyo tu yale uliyopanda bali pia matunda ya mizabibu.