1 Haya ni maneno ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu aliwaamuru Mose kufanya na Waisraeli katika nchi ya Moabu, licha ya agano Mwenyezi-Mungu alilofanya nao mlimani Horebu.
2 Mose aliwaita pamoja Waisraeli wote akawaambia, “Mliona nyinyi wenyewe jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomtendea mfalme wa Misri, maofisa, watumishi wake na nchi yake yote.
3 Mliona maafa makubwa, ishara na maajabu aliyotenda.
4 Lakini mpaka leo Mwenyezi-Mungu hajawapa akili ya kuelewa, macho ya kuona, wala masikio ya kusikia!
5 “Kwa muda wa miaka arubaini, mimi niliwaongoza jangwani, nguo zenu mlizovaa hazikuchakaa wala viatu vyenu havikuchakaa miguuni mwenu.
6 Hamkula mkate wala kunywa divai au kileo chochote kile, mpate kujua kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu.