22 “Hizi ndizo amri Mwenyezi-Mungu alizowaambieni nyote kwa sauti kubwa kutoka katika moto na lile wingu zito na giza nene. Aliwaambieni mlipokuwa mmekusanyika kule mlimani na hakuongeza hapo amri nyingine. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, akanipatia.
23 “Wakati mliposikia hiyo sauti kutoka katikati ya lile giza, juu ya ule mlima uliokuwa unawaka moto, viongozi wote wa makabila yenu na wazee walinijia
24 wakasema, ‘Sikiliza! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametufunulia utukufu na ukuu wake; tumeisikia sauti yake kutoka katikati ya ule moto. Leo hivi tumemwona Mungu akiongea na binadamu, naye binadamu badala ya kufa akaendelea kuishi!
25 Lakini ya nini kujitia katika hatari ya kufa kwa kuteketezwa na ule moto mkubwa? Tukiisikia tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tutakufa!
26 Je, ni binadamu gani aliyepata kumsikia Mungu aliye hai akiongea kutoka katikati ya moto kama tulivyomsikia sisi halafu akaweza kubaki hai?
27 Heri wewe Mose uende karibu, ukasikilize yote atakayosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kisha uje kutuambia mambo hayo yote atakayokuambia. Sisi tutayasikiliza na kuyatekeleza’.
28 “Mwenyezi-Mungu alisikia maneno yenu hayo, akaniambia ‘Nimesikia maneno waliyokuambia watu hawa; yote waliyosema ni sawa.