14 Mtabarikiwa kuliko watu wengine wote ulimwenguni. Miongoni mwenu hakutakuwa na mwanamume wala mwanamke tasa.
15 Mwenyezi-Mungu atawaondoleeni magonjwa yote na hamtapatwa na magonjwa yoyote ya kutisha kama yaliyowapata huko Misri, lakini atawapa maadui zenu magonjwa hayo.
16 Angamizeni taifa lolote ambalo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; atalitia mikononi mwenu, wala msilionee huruma. Msiabudu miungu yao, kwani jambo hili litakuwa mtego kwenu.
17 “Msijisemee mioyoni mwenu: ‘Watu hawa ni wengi kuliko sisi, twawezaje kuwafukuza nchini?’
18 Msiwaogope, kumbukeni vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyomtendea Farao na nchi nzima ya Misri.
19 Kumbukeni maradhi mabaya mliyoyaona kwa macho yenu, miujiza na maajabu na nguvu kubwa na uwezo mkuu, ambavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; alitumia kuwakomboa; hivyo ndivyo atakavyowatenda watu mnaowaogopa.
20 Zaidi ya hayo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atapeleka mavu kati yao na kuwaangamiza wale ambao watawatoroka ili kujificha.