1 Anayetafuta yake tu hujitenga na wenzake;hukasirika akipewa shauri lolote jema.
2 Mpumbavu hapendezwi na busara;kwake cha maana ni maoni yake tu.
3 Ajapo mwovu huja pia dharau;pamoja na aibu huja fedheha.
4 Maneno yaweza kuwa chemchemi ya hekima;yenye kilindi kama bahari, kama kijito kinachobubujika.
5 Si vizuri kumpendelea mtu mwovu,na kumnyima haki mtu mwadilifu.
6 Maneno ya mpumbavu huleta ugomvi;kila anachosema husababisha adhabu.
7 Kinywa cha mpumbavu humwangamiza mwenyewe;mdomo wake ni mtego wa kumnasa yeye mwenyewe.
8 Maneno ya msengenyaji ni kama kitoweo kitamu;ambacho hushuka moja kwa moja mpaka tumboni.
9 Mtu mvivu kazini mwakeni ndugu yake mharibifu.
10 Jina la Mwenyezi-Mungu ni mnara imara;mwadilifu huukimbilia akawa salama.
11 Lakini tajiri hudhani mali ni ngome yake;anafikiri hayo ni ukuta mrefu unaomlinda.
12 Majivuno ya moyoni huleta maangamizi,lakini unyenyekevu huleta heshima.
13 Kujibu kabla ya kusikilizani upumbavu na jambo la aibu.
14 Roho ya mtu huweza kustahimili ugonjwa,lakini ukiwa umevunjika moyo, utastahimilije?
15 Mtu mwenye akili hujipatia maarifa,sikio la mwenye busara hutafuta maarifa.
16 Zawadi humfungulia mtu milango;huweza kumfikisha mtu mbele ya mkuu.
17 Ajiteteaye kwanza huonekana msema kweli,mpaka hapo mpinzani wake atakapoanza kumhoji.
18 Kura hukomesha ubishi;huamua kati ya wakuu wanaopingana.
19 Ndugu aliyeudhiwa ni mgumu kuliko mji wa ngome;magomvi hubana kama makufuli ya ngome.
20 Maneno ya mtu yaweza kumshibisha;hutosheka kwa matokeo ya maneno yake.
21 Ulimi una nguvu ya kufanya hai na kuua;wanaopenda kuutumia watakula matunda yake.
22 Anayempata mke amepata bahati njema;hiyo ni fadhili kutoka kwa Mwenyezi-Mungu.
23 Maskini huomba kwa unyenyekevu,bali tajiri hujibu kwa ukali.
24 Marafiki wengi waweza kumwangusha mtu,lakini wapo marafiki waaminifu kuliko ndugu.