Methali 19 BHN

1 Afadhali maskini aishiye kwa unyofu,kuliko mtu mpotovu wa maneno na mpumbavu.

2 Haifai mtu kuwa bila akili;mwenda harakaharaka hujikwaa.

3 Mtu akijiangamiza kwa upumbavu wake,huielekeza hasira yake dhidi ya Mwenyezi-Mungu.

4 Mali huvuta marafiki wengi wapya,lakini maskini huachwa bila rafiki.

5 Shahidi mwongo hataacha kuadhibiwa;asemaye uongo hataepa adhabu.

6 Watu wengi hujipendekeza kwa wakuu;kila mtu hutaka kuwa rafiki ya mtu mkarimu.

7 Maskini huchukiwa na ndugu zake;marafiki zake ndio zaidi: Humkimbia!Hata awabembeleze namna gani hatawapata.

8 Ajipatiaye hekima anaipenda nafsi yake;anayezingatia busara atastawi.

9 Shahidi mwongo hatakosa kuadhibiwa;asemaye uongo ataangamia.

10 Haifai kwa mpumbavu kuishi kwa anasa,tena ni vibaya zaidi mtumwa kuwatawala wakuu.

11 Mwenye busara hakasiriki upesi;kusamehe makosa ni fahari kwake.

12 Ghadhabu ya mfalme ni kama ngurumo ya simba,lakini wema wake ni kama umande juu ya majani.

13 Mtoto mpumbavu ni balaa kwa baba yake;na ugomvi wa mke ni kama matone ya mvua yasiyoisha.

14 Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa wazee wake,lakini mke mwenye busara hutoka kwa Mwenyezi-Mungu.

15 Uzembe ni kama usingizi mzito;mtu mvivu atateseka kwa njaa.

16 Anayeshika amri anasalimisha maisha yake;anayepuuza agizo atakufa.

17 Anayemsaidia maskini anamkopesha Mwenyezi-Mungu;Mwenyezi-Mungu atamlipa kwa tendo lake jema.

18 Mrudi mwanao kungali bado na tumaini,lakini usimwadhibu kiasi cha kumwangamiza.

19 Mtu wa hasira kali lazima apate adhabu;ukimwachia mara moja itakubidi kumwachia tena.

20 Sikiliza shauri na kupokea mafundisho,upate hekima ya kukufaa siku zijazo.

21 Kichwani mwa mtu mna mipango mingi,lakini anachokusudia Mwenyezi-Mungu ndicho kitakachofanyika.

22 Kinachotakiwa kwa mtu ni uaminifu;afadhali mtu maskini kuliko mtu mwongo.

23 Kumcha Mwenyezi-Mungu kunaleta uhai;amchaye hujaliwa pumziko la kutosheleza,wala hatapatwa na baa lolote.

24 Mvivu ni kama mtu atiaye mkono katika sahani ya chakula,lakini hana nguvu ya kuuinua hadi mdomoni.

25 Mwadhibu mwenye mzaha naye mjinga atapata akili;mwonye mwenye busara naye atapata maarifa.

26 Anayemdhulumu baba yake na kumfukuza mama yake,ni mtoto asiyefaa na mpotovu.

27 Mwanangu, ukiacha kusikiliza mafundisho,utapotea mara mbali na maneno ya hekima.

28 Shahidi asiyefaa kitu huidhihaki haki;na kinywa cha mwovu hubugia uovu.

29 Adhabu iko tayari kwa wenye mzaha,mijeledi imetayarishwa kuchapa migongo ya wapumbavu.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31