Methali 8 BHN

Wito wa Hekima

1 Sikilizeni! Hekima anaita!Busara anapaza sauti yake!

2 Juu penye mwinuko karibu na njia,katika njia panda ndipo alipojiweka.

3 Karibu na malango ya kuingilia mjini,mahali wanapoingia watu anaita kwa sauti:

4 “Enyi watu wote, nawaita nyinyi!Wito wangu ni kwa ajili ya binadamu.

5 Enyi wajinga, jifunzeni kuwa na akili;sikilizeni kwa makini enyi wapumbavu.

6 Sikilizeni maana nitakachosema ni jambo muhimu;midomoni mwangu mtatoka mambo ya adili.

7 Kinywa changu kitatamka kweli tupu;uovu ni chukizo midomoni mwangu.

8 Kinywa changu kitatamka maneno ya kweli,udanganyifu ni haramu midomoni mwangu.

9 Kwa mtu mwelewa kila kitu ni wazi,kwa mwenye maarifa yote ni sawa.

10 Chagua mafundisho yangu badala ya fedha;na maarifa badala ya dhahabu safi.

11 “Mimi Hekima nina thamani kuliko johari;chochote unachotamani hakiwezi kulingana nami.

12 Mimi Hekima ninao ujuzi;ninayo maarifa na busara.

13 Kumcha Mwenyezi-Mungu ni kuchukia uovu.Nachukia kiburi, majivuno na maisha mabaya;nachukia na lugha mbaya.

14 Nina uwezo wa kushauri na nina hekima.Ninao ujuzi na nina nguvu.

15 Kwa msaada wangu wafalme hutawala,watawala huamua yaliyo ya haki.

16 Kwa msaada wangu viongozi hutawala,wakuu na watawala halali.

17 Nawapenda wale wanaonipenda;wanaonitafuta kwa bidii hunipata.

18 Utajiri na heshima viko kwangu,mali ya kudumu na fanaka.

19 Matunda yangu ni mazuri kuliko dhahabu safi,faida yangu yashinda ile ya fedha bora.

20 Natembea katika njia ya uadilifu;ninafuata njia za haki.

21 Mimi huwatajirisha wanaonipenda,huzijaza tele hazina zao wanipendao.

22 “Mwenyezi-Mungu aliniumba mwanzoni mwa kazi yake,zama za zama kabla ya kuwako kitu chochote.

23 Nilifanywa mwanzoni mwa nyakati,nilikuwako kabla ya dunia kuanza.

24 Nilizaliwa kabla ya vilindi vya bahari,kabla ya chemchemi zibubujikazo maji.

25 Kabla ya milima haijaumbwa,na vilima kusimamishwa mahali pake,mimi nilikuwako tayari.

26 Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake,wala chembe za kwanza za mavumbi ya dunia.

27 Nilikuwako wakati alipoziweka mbingu,wakati alipopiga duara juu ya bahari;

28 wakati alipoimarisha mawingu mbinguni,alipozifanya imara chemchemi za bahari;

29 wakati alipoiwekea bahari mpaka wake,maji yake yasije yakavunja amri yake;wakati alipoiweka misingi ya dunia.

30 Nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi,nilikuwa furaha yake kila siku,nikishangilia mbele yake daima,

31 nikifurahia dunia na wakazi wake,na kupendezwa kuwa pamoja na wanadamu.

32 “Sasa basi wanangu, nisikilizeni:Heri wale wanaofuata njia zangu.

33 Sikilizeni mafunzo mpate hekima,wala msiyakatae.

34 Heri mtu anayenisikiliza,anayekaa kila siku mlangoni pangu,anayekesha karibu na milango yangu.

35 Anayenipata mimi amepata uhai,amepata upendeleo kwa Mwenyezi-Mungu.

36 Asiyenipata anajidhuru mwenyewe;wote wanaonichukia wanapenda kifo.”

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31