1 Hizi ni methali za Solomoni mfalme wa Israeli, mwana wa Daudi.
2 Methali hizi zawapatia watu hekima na nidhamu; zawafanya waelewe maneno ya busara,
3 zawafanya kuwa na nidhamu, utaratibu, uadilifu, haki na kutenda kwa usawa.
4 Huwapatia wajinga werevu na vijana maarifa na hadhari.
5 Mwenye hekima azisikie na kuongeza elimu yake, naye mwenye busara apate mwongozo.
6 Mtu aelewe methali na mifano, maneno ya wenye hekima na vitendawili vyao.
7 Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa maarifa,lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu.
8 Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako,wala usiyapuuze mafundisho ya mama yako;
9 hayo yatakupamba kilemba kichwani pako,kama mkufu shingoni mwako.
10 Mwanangu, usikubali kushawishiwa na wenye dhambi.
11 Wakisema: “Twende tukamvizie mtu na kumuua;njoo tukawashambulie wasio na hatia!
12 Tutawameza kama Kuzimu wakiwa hai,watakuwa kama wale washukao Shimoni.
13 Tutajitwalia mali zote za thamani,nyumba zetu tutazijaza nyara.
14 Njoo ushirikiane nasi,vyote tutakavyopata tutagawana.”
15 Wewe mwanangu usiandamane nao,uzuie mguu wako usifuatane nao.
16 Maana wao wako mbioni kutenda maovu,haraka zao zote ni za kumwaga damu.
17 Mtego utegwao huku ndege anaona,mtego huo wategwa bure.
18 Wao huvizia na kujiangamiza wao wenyewe,hutega mtego wa kujinasa wao wenyewe.
19 Ndivyo zilivyo njia za waishio kwa ukatili;ukatili huyaangamiza maisha ya wakatili.
20 Hekima huita kwa sauti barabarani,hupaza sauti yake sokoni;
21 huita juu ya kuta,hutangaza penye malango ya mji:
22 “Enyi wajinga! Mpaka lini mtapenda kuwa wajinga?Mpaka lini wenye dharau watafurahia dharau zao,na wapumbavu kuchukia maarifa?
23 Sikilizeni maonyo yangu;nitawamiminia mawazo yangu,nitawajulisha maneno yangu.
24 Kwa kuwa nimewaita mkakataa kusikiliza,nimewapungia mkono mje mkakataa,
25 mkapuuza mashauri yangu yote,wala hamkuyajali maonyo yangu,
26 nami pia nitayachekelea maafa yenu,nitawadhihaki mnapokumbwa na hofu,
27 hofu itakapowakumba kama tufani,maafa yenu yatakapowavamia kama kimbunga,wakati udhia na dhiki vitakapowapata.
28 Hapo ndipo mtakaponiita lakini sitaitika;mtanitafuta kwa bidii lakini hamtanipata.
29 Kwa kuwa mliyachukia maarifa,wala hamkuchagua kumcha Mwenyezi-Mungu;
30 maadamu mlikataa shauri langu,mkayapuuza maonyo yangu yote;
31 basi, mtakula matunda ya mienendo yenu,mtavimbiwa kwa hila zenu wenyewe.
32 Maana wajinga hujiua kwa ukaidi wao,wapumbavu hujiangamiza kwa kujiamini kwao.
33 Lakini kila anisikilizaye atakaa salama,atatulia bila kuogopa mabaya.”