Methali 28 BHN

1 Waovu hukimbia japo hawafukuzwi na mtu,lakini waadilifu ni hodari kama simba.

2 Taifa la fujo huzusha viongozi wengi,lakini kwa kiongozi mmoja mwenye akili na maarifa huwa na utengemano

3 Mtu mhitaji anayewadhulumu maskini,amefanana na mvua kubwa inayoharibu mimea.

4 Watu wanaovunja sheria huwasifu waovu,lakini wanaoishika sheria hupingana nao.

5 Waovu hawajui maana ya haki,lakini wamchao Mwenyezi-Mungu wanaielewa kabisa.

6 Afadhali maskini aishiye kwa unyofu,kuliko tajiri aishiye kwa upotovu.

7 Mtoto ashikaye sheria ni mwenye hekima,lakini rafiki wa walafi humwaibisha baba yake.

8 Aongezaye mali yake kwa riba na kutoza faidaanamkusanyia mwingine mwenye kuwahurumia maskini.

9 Anayekataa kuisikia sheria,huyo hata sala yake ni chukizo kwa Mungu.

10 Anayemshawishi mtu mwema kutenda mabaya,ataanguka katika shimo lake mwenyewe.Wasio na hatia wamewekewa mema yao.

11 Tajiri hujiona mwenyewe kuwa mwenye hekima,lakini maskini mwenye busara atamfichua.

12 Watu wema wakipata madaraka maisha hufana,lakini waovu wakitawala watu hujificha.

13 Afichaye makosa yake hatafanikiwa;lakini anayeungama na kuyaacha atapata rehema.

14 Heri mtu amchaye Mwenyezi-Mungu daima;lakini mkaidi wa moyo ataangukia maafa.

15 Mtawala mwovu anayewatawala maskini,ni kama simba angurumaye au dubu anayeshambulia.

16 Mtawala asiye na akili ni mdhalimu mkatili;lakini achukiaye mali ya udanganyifu atatawala muda mrefu.

17 Mtu anayelemewa na hatia ya kuua mtu,atakuwa mkimbizi mpaka kaburini;mtu yeyote na asijaribu kumzuia.

18 Aishiye kwa unyofu atasalimishwa,lakini mdanganyifu ataanguka kabisa.

19 Anayelima shamba lake atapata chakula kingi,bali anayefuata yasiyofaa atapata umaskini tele.

20 Mtu mwaminifu atapata baraka tele,lakini mwenye pupa ya kuwa tajiri hataepa adhabu.

21 Si vizuri kumbagua mtu;watu hufanya mabaya hata kwa kipande cha mkate.

22 Mtu bahili hukimbilia mali,wala hajui kwamba ufukara utamjia.

23 Amwonyaye mwenzake hatimaye hupata mema zaidi,kuliko yule anayembembeleza kwa maneno matamu.

24 Anayeiba mali ya baba yake au mama yake, akasema si kosa,hana tofauti yoyote na wezi wengine.

25 Mchoyo huchochea ugomvi,lakini anayemtegemea Mwenyezi-Mungu atafanikiwa.

26 Anayetegemea akili yake mwenyewe ni mpumbavu;lakini anayeishi kwa hekima atakuwa salama.

27 Aliye mkarimu kwa maskini hatatindikiwa kitu,lakini anayekataa kuwaangalia atalaaniwa kwa wingi.

28 Waovu wakitawala watu hujificha,lakini wakiangamia, waadilifu huongezeka.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28 29 30 31