13 Afichaye makosa yake hatafanikiwa;lakini anayeungama na kuyaacha atapata rehema.
14 Heri mtu amchaye Mwenyezi-Mungu daima;lakini mkaidi wa moyo ataangukia maafa.
15 Mtawala mwovu anayewatawala maskini,ni kama simba angurumaye au dubu anayeshambulia.
16 Mtawala asiye na akili ni mdhalimu mkatili;lakini achukiaye mali ya udanganyifu atatawala muda mrefu.
17 Mtu anayelemewa na hatia ya kuua mtu,atakuwa mkimbizi mpaka kaburini;mtu yeyote na asijaribu kumzuia.
18 Aishiye kwa unyofu atasalimishwa,lakini mdanganyifu ataanguka kabisa.
19 Anayelima shamba lake atapata chakula kingi,bali anayefuata yasiyofaa atapata umaskini tele.