1 Anayeonywa mara nyingi akawa mkaidi,ataangamia ghafla asipone tena.
2 Waadilifu wakitawala watu hufurahi,lakini waovu wakitawala watu hulalamika.
3 Apendaye hekima humfurahisha baba yake;lakini aandamanaye na malaya hufuja mali yake.
4 Mfalme akitumia haki huipatia nchi uthabiti,lakini akipenda hongo taifa huangamia.
5 Mwenye kumbembeleza jirani yake,anatega mtego wa kujinasa mwenyewe.
6 Mtu mbaya hunaswa kwa kosa lake,lakini mtu mwadilifu huimba na kufurahi.
7 Mwadilifu anajua haki za maskini,lakini mtu mwovu hajui mambo hayo.