1 Sanbalati aliposikia kuwa tumeanza kazi ya kuujenga upya ukuta, alikasirika sana, akaanza kutukebehi,
2 mbele ya rafiki zake na majeshi ya Wasamaria, akisema, “Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, kusudi lao ni kuujenga upya mji? Je, watatoa tambiko? Wanaweza kumaliza kazi kwa siku moja tu? Je, wataweza kufanya mawe yaliyorundikana kwenye takataka na kuteketea, yafae kujengea?”
3 Tobia, Mwamoni, aliyekuwa akisimama karibu naye, alitilia mkazo akisema, “Wanajenga nini? Mbweha akipanda juu yake, atabomoa huo ukuta wao wa mawe!”
4 Ndipo nikamwomba Mungu nikisema, “Ee Mungu wetu, sikia wanavyotukebehi; urudishe dharau yao juu yao wenyewe na uwaache watekwe na kuchukuliwa mateka katika nchi ya kigeni.
5 Kamwe usiwasamehe hatia yao, wala dhambi yao kamwe usiisamehe; kwani wamekukasirisha mbele ya wajenzi.”
6 Lakini tuliendelea na ujenzi wa ukuta mpaka ukafikia nusu yake kwa sababu watu walikuwa wamedhamiria kwa dhati.