1 Baada ya muda kulitokea malalamiko miongoni mwa watu, wanaume kwa wanawake, wakiwalalamikia ndugu zao Wayahudi.
2 Kulitokea waliosema, “Tafadhali tupatie nafaka tule ili tuweze kuishi kwa kuwa sisi, wana wetu na binti zetu tu wengi.”
3 Na wengine wakalalamika, “Tumeweka rehani mashamba yetu, mizabibu yetu hata na nyumba zetu ili kupata nafaka kwa sababu ya njaa.”
4 Tena kukawa na hata wale, waliolalamika, wakisema, “Ili kulipa kodi ya mfalme juu ya mashamba na mizabibu yetu, ilitubidi tukope fedha.
5 Lakini sisi ni sawa na Wayahudi wengine; watoto wetu ni sawa na watoto wao. Hata hivyo, tunawalazimisha watoto wetu kuwa watumwa. Baadhi ya binti zetu tayari ni watumwa. Hatuna uwezo wa kuzuia jambo hili kwani mashamba yetu na mizabibu yetu yameporwa na watu wengine.”
6 Niliposikia malalamiko yao, nilikasirika sana.
7 Nikaamua kuchukua hatua. Nikawashutumu wakuu na maofisa, nikawaambia, “Mnawatoza riba ndugu zenu.”