1 Watu wa kabila la Efraimu walikusanyika, wakavuka mto Yordani wakafika huko Zafoni. Kisha wakamwambia Yeftha, “Kwa nini hukutuita tuende pamoja nawe kupigana na Waamoni? Sasa tutaichoma nyumba yako nawe mwenyewe ndani yake.”
2 Yeftha akawaambia, “Mimi pamoja na watu wangu tulikuwa na uadui mkubwa na Waamoni. Niliwaombeni mnisaidie lakini hamkuja kuniokoa.
3 Nilipoona kwamba hamkuja kuniokoa, nilikwenda, roho mkononi, kupigana na Waamoni, naye Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu. Kwa nini sasa mnakuja kupigana na mimi?”
4 Basi, Yeftha akakusanya watu wote wa Gileadi, akapigana na watu wa Efraimu. Watu wa Gileadi wakawashinda watu wa Efraimu. Hawa Waefraimu ndio hao waliokuwa wamesema: “Nyinyi watu wa Gileadi ni wakimbizi wa kabila la Efraimu mliotoka katika kabila la Efraimu mkaenda kwa kabila la Manase.”
5 Kisha watu wakavishika vivuko vya mto Yordani ili kuiziba njia ya watu wa Efraimu. Kila mara alipotokea mkimbizi akaomba kupita huko, watu wa Gileadi walimwuliza, “Je, wewe ni Mwefraimu?” Na kama alijibu, “La,”
6 walimwambia: “Haya tamka neno ‘Shibolethi’” lakini yeye hutamka “Sibolethi,” kwa sababu hakuweza kulitamka sawasawa. Hapo, walimkamata, wakamuua huko kwenye vivuko vya mto Yordani. Watu 42,000 wa Efraimu walipoteza maisha yao wakati huo.
7 Yeftha alikuwa mwamuzi katika Israeli kwa miaka sita. Kisha akafariki, akazikwa huko Gileadi katika mji wake.