1 Baada ya muda fulani, wakati wa mavuno ya ngano, Samsoni alichukua mwanambuzi, akaenda kumtembelea mkewe. Akamwambia baba mkwe wake kwamba anataka kumwona mke wake chumbani mwake. Lakini baba mkwe hakumruhusu,
2 akamwambia, “Mimi nilidhani ulimchukia kabisa. Kwa hiyo nilimwoza rafiki yako. Hata hivyo, dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye. Tafadhali, umwoe huyo badala yake.”
3 Samsoni akamwambia, “Safari hii sitakuwa na lawama kwa yale nitakayowatendea Wafilisti.”
4 Basi, Samsoni akaenda, akawakamata mbweha 300 na akawafunga mikia yao pamoja wawiliwawili. Kisha akaweka mwenge katika kila jozi ya mbweha.
5 Halafu akaiwasha hiyo mienge na kuwaachilia hao mbweha ambao waliingia kwenye mashamba ya Wafilisti na kuteketeza miganda ya ngano na pia ngano iliyokuwa bado haijavunwa hata na mashamba ya mizeituni.