11 Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.”
12 Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.”
13 Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni.
14 Alipofika Lehi, Wafilisti walimwendea mbio huku wakipiga kelele. Ghafla roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Samsoni kwa nguvu na zile kamba walizomfunga mikononi mwake zikakatika kama kitani kilichoshika moto, navyo vifungo vikaanguka chini.
15 Samsoni akapata utaya mbichi wa punda, akautumia kuwaua watu 1,000.
16 Kisha Samsoni akasema,“Kwa utaya wa punda,nimeua watu elfu moja.Kwa utaya wa punda,nimekusanya marundo ya maiti.”
17 Alipomaliza kusema, akatupa utaya huo. Mahali hapo pakaitwa Ramath-lehi, yaani mlima wa utaya.