7 Samsoni akawaambia hao Wafilisti, “Kama hayo ndiyo mliyoyafanya, naapa kwamba sitaondoka mpaka nimelipiza kisasi.”
8 Basi, akawashambulia vikali na kuwaua wengi. Kisha akaenda kuishi katika pango la mwamba wa Etamu.
9 Wafilisti wakaja, wakapiga kambi yao nchini Yuda na kuushambulia mji wa Lehi.
10 Watu wa Yuda wakawauliza, “Kwa nini mmekuja kutushambulia?” Nao wakawajibu, “Tumekuja ili tumfunge Samsoni na kumtendea kama alivyotutendea.”
11 Basi, watu 3,000 wa Yuda wakamwendea Samsoni pangoni mwa mwamba wa Etamu wakamwambia, “Je, hujui kwamba Wafilisti wanatawala juu yetu? Tazama basi, mkosi uliotutendea!” Samsoni akawajibu, “Kama walivyonitendea ndivyo nilivyowatendea.”
12 Wakamwambia, “Tumekuja kukufunga ili tukutie mikononi mwao.” Samsoni akawaambia, “Niapieni kwamba nyinyi wenyewe hamtaniua.”
13 Nao wakamwambia, “Sisi hatutakuua ila tutakufunga tu na kukutia mikononi mwao.” Basi, wakamfunga kwa kamba mbili mpya na kumtoa humo pangoni.