13 Kisha jumuiya nzima ikawapelekea ujumbe wa amani watu wa kabila la Benyamini ambao walikuwa kwenye mwamba wa Rimoni.
14 Wanaume hao wa kabila la Benyamini wakawarudia hao wenzao wakati huohuo. Basi wakapewa wale wanawake ambao walikuwa wamesalimishwa huko Yabesh-gileadi. Lakini wanawake hao hawakuwatosha.
15 Waisraeli wakawaonea huruma watu wa kabila la Benyamini, maana Mwenyezi-Mungu alisababisha kuweko na mwanya katika Israeli.
16 Kisha wazee wa jumuiya nzima wakasema, “Sasa tutafanya nini ili kuwapatia wanawake hao wanaume waliosalia kwa vile wanawake wote wa kabila la Benyamini waliangamia?
17 Lazima wanaume waliosalia wa kabila la Benyamini wapewe wanawake ili waendeleze kabila, na hivyo kusipotee kabila lolote katika Israeli.
18 Lakini hatuwezi kuwatoa binti zetu wawe wake zao, maana tulikwisha apa kwamba mtu yeyote atakayemwoza binti yake kwa mwanamume wa kabila la Benyamini alaaniwe.”
19 Basi wakakumbuka kwamba sikukuu ya Mwenyezi-Mungu iliyofanyika kila mwaka huko Shilo, mji ulio kaskazini ya Betheli, kwenye njia kuu itokayo Betheli kwenda Shekemu, ilikuwa inakaribia.