7 Hao makuhani wazawa wa Aroni watazipanga kuni juu ya madhabahu na kuwasha moto.
8 Kisha makuhani hao watachukua vile vipande vya nyama, kichwa na mafuta, na kuviweka juu ya kuni juu ya madhabahu.
9 Lakini matumbo na miguu ya mnyama huyo mtu ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza sadaka yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
10 “Kama sadaka yake ya kuteketezwa ataitoa katika kundi la kondoo au mbuzi, basi, atachagua dume asiye na dosari.
11 Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu, mbele ya Mwenyezi-Mungu, hao makuhani, wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu pande zake zote.
12 Kisha huyo mtu atamkata vipandevipande, akivitenga kichwa pamoja na mafuta yake, na kuhani ataviweka kwenye moto juu ya madhabahu.
13 Lakini matumbo na miguu yake ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.