14 Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na kunyunyiza kwa kidole chake upande wa mashariki juu ya kiti cha rehema kisha atainyunyizia mbele ya sanduku la agano mara saba kwa kidole chake.
15 “Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele.
16 Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi.
17 Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje.
18 Kisha atatoka na kwenda kwenye madhabahu iliyo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuifanyia ibada ya upatanisho. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na ya yule mbuzi na kuzipaka pembe za madhabahu pande zote.
19 Atainyunyizia madhabahu hiyo damu kwa kidole chake mara saba na hivyo kuiweka wakfu na kuitakasa unajisi wote wa watu wa Israeli.
20 “Baada ya Aroni kumaliza kupatakasa mahali patakatifu, hema la mkutano na madhabahu, ndipo atamtoa yule beberu kwa ajili ya Azazeli, akiwa hai.