3 Sehemu inayobaki ya sadaka hiyo ni ya makuhani. Hiyo ni sehemu takatifu kabisa ya sadaka anayotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto.
4 “Kama mtu anamtolea Mungu sadaka ya nafaka iliyookwa jikoni, hiyo itakuwa ya mikate isiyotiwa chachu ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni, au ya mikate myembamba isiyo na chachu na isiyopakwa mafuta.
5 Iwapo sadaka unayotoa ni ya mkate uliookwa kwenye kikaango, hiyo itakuwa ya unga laini uliochanganywa na mafuta ya zeituni lakini bila chachu.
6 Mikate hiyo itakatwakatwa na kumiminiwa mafuta; hiyo ni sadaka ya nafaka.
7 Kama sadaka unayotoa ni ya mikate iliyopikwa katika sufuria, hiyo itakuwa ya unga laini na imetiwa mafuta.
8 Utaleta sadaka ya nafaka iliyotengenezwa kwa vitu hivyo mbele ya Mwenyezi-Mungu; na kuhani ataipeleka kwenye madhabahu.
9 Kuhani atachukua sehemu ya sadaka hiyo ikiwa ni sadaka ya ukumbusho na kuiteketeza juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.