25 “Kama ndugu yako anakuwa maskini, akauza ardhi yake, basi, ndugu yake wa karibu mwenye jukumu la kuikomboa, ataikomboa.
26 Ikiwa mtu huyo hana ndugu mwenye jukumu la kuikomboa, lakini baadaye akawa tajiri na kupata uwezo wa kuikomboa ardhi yake,
27 basi, atahesabu miaka inayohusika tangu alipoiuza na kulipa gharama zake; na yule mtu aliyeinunua ni lazima amrudishie.
28 Lakini ikiwa hana uwezo wa kuikomboa, basi, itabaki mikononi mwa yule aliyeinunua mpaka mwaka wa sikukuu ya ukumbusho wa miaka hamsini. Katika mwaka huo, ni lazima mali hiyo iachiliwe na kurudishiwa yule mtu aliyeiuza.
29 “Kama mtu akiuza nyumba yake ya kuishi iliyo ndani ya mji uliojengewa ukuta, ataweza kuikomboa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu alipoiuza. Kwa mwaka huo mzima atakuwa na haki ya kuikomboa.
30 Kama nyumba iliyo katika mji uliojengewa ukuta haikukombolewa kwa muda wa mwaka mmoja, basi, itakuwa mali ya yule aliyeinunua milele katika vizazi vyao vyote; wala haitarudishwa katika mwaka wa sikukuu ya kukumbuka miaka hamsini.
31 Lakini nyumba za vijiji ambavyo havikuzungushiwa ukuta zitakuwa chini ya sheria ileile ya ardhi; nyumba hizo zinaweza kukombolewa katika mwaka mmoja lakini ni lazima zirudishwe kwa wenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini.