31 Lakini nyumba za vijiji ambavyo havikuzungushiwa ukuta zitakuwa chini ya sheria ileile ya ardhi; nyumba hizo zinaweza kukombolewa katika mwaka mmoja lakini ni lazima zirudishwe kwa wenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini.
32 Hata hivyo, nyumba zilizomo katika miji wanayomiliki Walawi zinaweza kukombolewa wakati wowote.
33 Ikiwa mmoja wa Walawi haitumii haki yake ya kukomboa, basi, nyumba iliyouzwa ni lazima irudishwe kwa mwenyewe katika mwaka wa kukumbuka miaka hamsini, kwani nyumba zilizomo katika miji wanayomiliki Walawi wamepewa kama sehemu yao kutoka kwa watu wa Israeli.
34 Lakini mashamba wanayomiliki Walawi kwa pamoja, yasiuzwe, kwani huo ni urithi wao wa kudumu.”
35 “Kama ndugu yako amekuwa maskini hata asiweze kujitunza mwenyewe akiwa pamoja nawe, ni lazima umtunze aendelee kuishi nawe; mtendee kama mgeni au msafiri aliye kwako.
36 Usimtake akulipe riba ya namna yoyote ile. Ila mche Mungu, naye ndugu yako apate kuishi pamoja nawe.
37 Usimkopeshe fedha kwa riba au kumpa chakula ili akulipe faida.