2 Shikeni sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
3 “Kama mkifuata masharti yangu na kuzishika amri zangu,
4 nitawanyeshea mvua wakati ufaao, nchi ipate kuzaa mavuno kwa wingi, nayo miti ya mashambani matunda yake.
5 Kupura nafaka kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu, na uvunaji zabibu mpaka wakati wa kupanda mbegu. Mtakuwa na chakula tele na kuishi kwa usalama nchini mwenu.
6 Nitawapeni amani nchini hata muweze kulala bila ya kuogopeshwa na chochote. Nitawaondoa wanyama wakali katika nchi na nchi yenu haitakumbwa na vita.
7 Mtawafukuza adui zenu na kuwaua kwa upanga.
8 Watano wenu watawafukuza adui 100 na 100 wenu watawafukuza adui 10,000. Adui zenu wataangamia mbele yenu kwa upanga.