17 Lakini nyama ya ng'ombe huyo, ngozi yake na mavi yake, akaviteketeza kwa moto nje ya kambi kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
18 Kisha, Mose akamleta kondoo dume wa sadaka ya kuteketezwa. Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo huyo.
19 Mose akamchinja na damu ya kondoo huyo akairashia madhabahu pande zake zote.
20 Alimkata huyo kondoo vipandevipande, akaviteketeza pamoja na kichwa chake na mafuta yake.
21 Baada ya matumbo na miguu kuoshwa kwa maji, Mose aliviteketeza vyote juu ya madhabahu pamoja na sehemu nyingine za huyo kondoo kama sadaka ya kuteketezwa. Hiyo ni sadaka itolewayo kwa moto, yenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. Mose alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
22 Kisha akamleta kondoo dume mwingine, kwa ajili ya kuweka wakfu. Aroni na wanawe wakaweka mikono yao juu ya kichwa cha kondoo huyo.
23 Mose akamchinja. Akachukua damu ya kondoo huyo na kumpaka Aroni kwenye ncha ya sikio lake la kulia, kidole gumba cha mkono wake wa kulia na cha mguu wake wa kulia.