8 Pamoja na vijiji vyote vilivyoizunguka miji hiyo hadi Baalath-beeri, (au Rama) ya Negebu. Hizo zote ni sehemu zilizopewa koo za kabila la Simeoni.
9 Kwa vile eneo lililopewa kabila la Yuda lilikuwa kubwa kuliko kabila hilo lilivyohitaji, sehemu ya eneo lake lilipewa kabila la Simeoni.
10 Kura ya tatu ilizipata koo za kabila la Zebuluni. Eneo lao lilienea hadi Saridi.
11 Kutoka huko mpaka wake ulikwenda magharibi hadi Mareali, ukapitia pembeni mwa Dabeshethi na kwenda kwenye kijito kilichoko mashariki ya Yokneamu.
12 Kutoka Saridi, mpaka huo ulielekea mashariki hadi kwenye mpaka wa Kisloth-tabori, na kutoka huko ukapita Daberathi hadi Yafia.
13 Kutoka Yafia uliendelea mashariki hadi Gath-heferi, Eth-kasini, na kuendelea hadi Rimoni ambako ulipanda kuelekea Nea.
14 Upande wa kaskazini mpaka uligeuka kuelekea Hanathoni na kuishia kwenye bonde la Yiftaheli.