15 Basi, Rahabu akawashusha hao watu kwa kamba kupitia dirishani, kwa kuwa nyumba yake ilikuwa imejengwa ikiambatana na ukuta wa mji wa Yeriko.
16 Akawaambia: “Nendeni mlimani mkajifiche huko ili wanaowafuatia wasiwakute. Kaeni huko kwa muda wa siku tatu, mpaka wanaowafuatia watakapokuwa wamerudi mjini, kisha mwende zenu.”
17 Hao watu wakamwambia, “Sisi tutalitimiza kabisa jambo ulilotufanya tuahidi kwa kiapo.
18 Tutakapokuja katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu kwenye dirisha ambalo umetuteremshia. Uwakusanye hapa kwako baba yako, mama yako na kaka zako na jamaa yote ya baba yako.
19 Lakini mtu yeyote akitoka nje ya nyumba yako na kwenda mitaani hatutakuwa na lawama juu ya kifo chake. Lakini kama mtu yeyote atakayekuwamo ndani ya nyumba yako akiguswa tu, basi lawama ya kifo chake itakuwa juu yetu.
20 Lakini kama ukimwambia mtu yeyote juu ya shughuli hii yetu, basi, sisi hatutabanwa na kiapo ulichotufanya tukuapie.”
21 Naye akawaambia “Na iwe jinsi mlivyosema.” Kisha akawaruhusu waende zao, nao wakaondoka. Naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani.