8 Kisha niliwaongoza hadi katika nchi ya Waamori ambao waliishi upande mwingine wa mto Yordani. Walipigana nanyi, lakini mimi niliwapeni ushindi juu yao mkawaangamiza na kuiteka nchi yao.
9 Naye Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akaja na kuwashambulia Waisraeli. Akamwalika Balaamu mwana wa Beori aje kuwalaani nyinyi.
10 Lakini mimi sikumsikiliza Balaamu, naye ikambidi kuwabariki, nami nikawaokoa nyinyi mikononi mwa Balaki.
11 Halafu mkavuka mto Yordani, mkafika Yeriko. Wakazi wa Yeriko walipigana nanyi, hali kadhalika na Waamori, Waperizi, Wakanaani, Wahiti, Wagirgashi, Wahivi na Wayebusi. Hao mimi nikawatia mikononi mwenu.
12 Nilituma manyigu mbele yenu ambayo yaliwatimua wafalme wawili wa Waamori. Hamkufanya haya kwa kupania mapanga wala pinde zenu.
13 “Niliwapeni mashamba ambayo hamkuwa mmeyalima, na miji ambayo hamkuijenga ambamo sasa mnaishi, na kula matunda ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuipanda.
14 “Sasa, basi, mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa moyo mnyofu na uaminifu. Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliiabudu ngambo ya mto Eufrate na nchini Misri. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu.