10 Nikaichukua ile fimbo yangu niliyoiita “Fadhili,” nikaivunja, kuonesha kwamba agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na watu wake limevunjwa.
11 Na agano hilo likavunjwa siku hiyohiyo. Wale wafanyabiashara ya kondoo waliokuwa wananiangalia, wakajua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa ameongea kwa matendo yangu.
12 Kisha nikawaambia, “Kama mnaona kuwa ni sawa, nilipeni ujira wangu; lakini kama mnaona sivyo, basi kaeni nao.” Basi, wakanipimia vipande thelathini vya fedha mshahara wangu.
13 Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Ziweke katika hazina ya hekalu.” Mshahara huo ulikuwa ni malipo halali kwa kazi yangu. Hivyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha, nikazitia katika hazina ya hekalu la Mwenyezi-Mungu.
14 Kisha nikaivunja ile fimbo yangu ya pili niliyoiita “Umoja;” na hivyo nikauvunja umoja kati ya Yuda na Israeli.
15 Mwenyezi-Mungu akaniambia tena, “Jifanye tena mchungaji, lakini safari hii uwe kama mchungaji mbaya!
16 Maana nitaleta nchini mchungaji asiyemjali kondoo anayeangamia, au kumtafuta kondoo anayetangatanga, au kumtibu aliyejeruhiwa wala kumlisha aliye hai: Bali atakula wale kondoo wanono, hata kwato zao.