2 Watu wa mji wa Betheli walikuwa wamewatuma Sharesa na Regem-meleki pamoja na watu wao kumwomba Mwenyezi-Mungu fadhili zake,
3 na kuwauliza makuhani wa hekalu la Mwenyezi-Mungu wa majeshi na manabii swali hili: “Je, tuendelee kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano kama tulivyofanya kwa muda wa miaka mingi sasa?”
4 Hapo, neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi likanijia:
5 “Waambie wakazi wote wa nchi na makuhani hivi: ‘Kwa muda wa miaka sabini iliyopita, nyinyi mmekuwa mkifunga na kuomboleza mnamo mwezi wa tano na wa saba. Je, mnadhani mlifunga kwa ajili yangu?
6 Je, mnapokula na kunywa, si mnakula na kunywa kwa ajili yenu wenyewe?’
7 Haya ndiyo mambo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu niliwaambieni kupitia kwa manabii wa hapo kwanza, wakati mji wa Yerusalemu ulikuwa umestawi na wenye wakazi tele, na wakati ambapo kulikuwa na wakazi wengi katika miji ya kandokando yake na katika eneo la Negebu na nyanda za Shefela.”
8 Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mimi Zekaria: