13 Enyi watu wa Yuda na watu wa Israeli! Wakati uliopita nyinyi mlionekana kuwa watu waliolaaniwa kati ya watu wa mataifa. Lakini sasa mimi nitawaokoeni, nanyi mtakuwa watu waliobarikiwa. Basi, msiogope tena, bali jipeni moyo!”
14 Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Kama nilivyokusudia kuwatendea nyinyi maovu kwa sababu wazee wenu walinikasirisha, na wala sikuwaonea huruma,
15 vivyo hivyo nimekusudia kuutendea wema mji wa Yerusalemu na watu wa Yuda. Basi, msiogope.
16 Hivi ndivyo mnavyopaswa kufanya: Kila mmoja wenu na amwambie mwenzake ukweli. Mahakama yenu daima na yatoe hukumu za haki ziletazo amani.
17 Mtu yeyote miongoni mwenu asikusudie kutenda uovu dhidi ya mwenzake, wala msiape uongo, maana nayachukia sana matendo hayo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
18 Neno la Mwenyezi-Mungu wa majeshi lilinijia mimi Zekaria:
19 “Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Siku za mfungo za mwezi wa nne, mwezi wa tano, mwezi wa saba na mwezi wa kumi, zitakuwa nyakati za furaha na shangwe; zitakuwa sikukuu za sherehe kwa watu wa Yuda. Basi, pendeni ukweli na amani.”