Mt. 8 SUV

Yesu Amtakasa mwenye Ukoma

1 Naye aliposhuka mlimani, makutano mengi walimfuata.

2 Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.

3 Yesu akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika.

4 Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao.

Yesu Amponya Mtumishi wa Afisa

5 Hata alipoingia Kapernaumu, akida mmoja alimjia,

6 akamsihi, akisema, Bwana, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza, anaumwa sana.

7 Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye.

8 Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.

9 Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya.

10 Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli.

11 Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;

12 bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

13 Naye Yesu akamwambia yule akida, Nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini. Mtumishi wake akapona saa ile ile.

Yesu Aponya Wengi Nyumbani kwa Petro

14 Hata Yesu alipofika nyumbani kwa Petro, akamwona mkwe wa Petro, mamaye mkewe, amelala kitandani hawezi homa.

15 Akamgusa mkono, homa ikamwacha; naye akaondoka, akawatumikia.

16 Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,

17 ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu,Na kuyachukua magonjwa yetu.

Watakaokuwa Wafuasi wa Yesu

18 Naye Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo.

19 Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata ko kote uendako.

20 Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake.

21 Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu.

22 Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

Yesu Atuliza Dhoruba

23 Akapanda chomboni, wanafunzi wake wakamfuata.

24 Kukawa msukosuko mkuu baharini, hata chombo kikafunikizwa na mawimbi; naye alikuwa amelala usingizi.

25 Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia.

26 Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga, enyi wa imani haba? Mara akaondoka, akazikemea pepo na bahari; kukawa shwari kuu.

27 Wale watu wakamaka wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?

Yesu Awaponya Wagadara Wenye Pepo

28 Naye alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile.

29 Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?

30 Basi, kulikuwako mbali nao kundi la nguruwe wengi wakilisha.

31 Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende, tukaingie katika lile kundi la nguruwe.

32 Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe; na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini.

33 Lakini wachungaji walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote na habari za wale wenye pepo pia.

34 Na tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28