Mt. 13 SUV

Mfano wa Mpanzi

1 Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari.

2 Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.

3 Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.

4 Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;

5 nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;

6 na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.

7 Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;

8 nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.

9 Mwenye masikio na asikie.

Sababu ya kusema kwa Mifano

10 Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?

11 Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.

12 Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

13 Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa.

14 Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema,Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa;Kutazama mtatazama, wala hamtaona.

15 Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito,Na kwa masikio yao hawasikii vema,Na macho yao wameyafumba;Wasije wakaona kwa macho yao,Wakasikia kwa masikio yao,Wakaelewa kwa mioyo yao,Wakaongoka, nikawaponya.

16 Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.

17 Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.

Maelezo ya Mfano wa Mpanzi

18 Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi.

19 Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.

20 Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha;

21 lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.

22 Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai.

23 Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.

Mfano wa Magugu katikati ya Ngano

24 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.

30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Mfano wa Punje ya Haradali

31 Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake;

32 nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.

Mfano wa Chachu

33 Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.

Matumizi ya Mifano

34 Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno;

35 ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,Nitafumbua kinywa changu kwa mifano,Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Yesu aelezea Mfano wa Magugu

36 Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.

37 Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;

38 lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;

39 yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.

40 Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.

41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,

42 na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

43 Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.

Mifano Mitatu

44 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.

45 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;

46 naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.

47 Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;

48 hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa.

49 Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki,

50 na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Hazina Mpya na ya Kale

51 Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.

52 Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.

53 Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

Kukataliwa kwa Yesu katika Nazareti

54 Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?

55 Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?

56 Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?

57 Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe.

58 Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21 22 23 24 25 26 27 28