6 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
7 Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia.
8 Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.
9 Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa BWANA amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.
10 Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.
11 Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani.
12 Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya BWANA, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo.