25 Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini.
26 Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya.
27 Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe.
28 Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika.
29 Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.
30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika.
31 Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli.