36 Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali po pote.
37 Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.
38 Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi.
39 Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi.
40 Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi.
41 Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena.
42 Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa BWANA, na kukushuhudia, kusema, Siku ile ya kutoka kwako ukienda mahali po pote, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema?