27 Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.
28 Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, BWANA asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, BWANA ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi BWANA.
29 Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.
30 Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani.
31 Watumwa wake wakamwambia, Angalia sasa, tumesikia ya kuwa wafalme wa nyumba ya Israeli ni wafalme wenye rehema; tafadhali, tuvae magunia viunoni, na kamba vichwani, tumtokee mfalme wa Israeli; labda atakuokoa roho yako.
32 Basi wakajifungia magunia viunoni, na kamba vichwani, wakamjia mfalme wa Israeli, wakasema, Mtumwa wako Ben-hadadi asema Roho yangu, nakusihi, iishi. Akasema, Je! Yu hai bado? Ni ndugu yangu yeye.
33 Wale watu wakaangalia sana, wakafanya haraka kulishika neno hilo kama ni nia yake, wakasema, Ndugu yako, Ben-hadadi. Akasema, Haya! Nendeni mkamlete. Ndipo Ben-hadadi akamtokea, naye akampandisha garini.