16 Nao wale walinzi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaangalia, na tazama, mkutano ule ulikuwa ukitoweka, na watu walikuwa wakienda huko na huko.
17 Ndipo Sauli akawaambia watu waliokuwa pamoja naye, Haya! Hesabuni sasa, mkaone ni nani aliyeondoka kwetu. Nao walipokwisha hesabu, tazama Yonathani na yeye aliyechukua silaha zake hawapo.
18 Basi Sauli akamwambia Ahiya, Lilete hapa sanduku la Mungu. Kwa kuwa hilo sanduku la Mungu wakati huo lilikuwapo pamoja na wana wa Israeli.
19 Ikawa Sauli alipokuwa katika kusema na kuhani, hayo makelele katika marago ya Wafilisti yakaendelea na kuzidi; basi Sauli akamwambia kuhani, Rudisha mkono wako.
20 Naye Sauli na watu wote waliokuwapo pamoja naye wakakusanyika, wakaenda vitani; na tazama, huko upanga wa kila mtu ulikuwa juu ya mwenziwe, kukawa fujo tele kabisa.
21 Basi na wale Waebrania waliokuwa pamoja na Wafilisti tangu zamani, wale waliopanda pamoja nao mpaka maragoni toka nchi iliyozunguka; watu hao nao wakageuka kuwa upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani.
22 Na vile vile watu wote wa Israeli waliokuwa wamejificha katika nchi ya milima milima ya Efraimu, waliposikia ya kwamba Wafilisti wamekimbia, hata hao nao wakawafuatia mbio vitani.