1 Kisha Daudi akatoka Nayothi huko Rama, akakimbia, akaenda kwa Yonathani, akasema mbele yake, Nimefanya nini? Uovu wangu ni nini? Dhambi yangu mbele ya baba yako ni nini, hata akaitaka roho yangu?
2 Naye akamwambia, Hasha! Hutakufa; angalia, baba yangu hatendi neno kubwa wala dogo bila kuifunulia mimi, na baba yangu ana sababu gani ya kunificha jambo hili? Sivyo usemavyo.
3 Daudi akaapa, akasema, Baba yako anajua sana ya kuwa nimeona kibali machoni pako, naye asema, Yonathani asilijue neno hili, asije akahuzunika; lakini ni kweli, aishivyo BWANA, na iishivyo roho yako, iko hatua moja tu kati ya mimi na mauti.
4 Ndipo Yonathani akamwambia Daudi, Kadiri roho yako itakavyo, nitakutendea.
5 Naye Daudi akamwambia Yonathani, Tazama, kesho ni mwandamo wa mwezi, nami hainipasi kukosa kuketi chakulani pamoja na mfalme; lakini niache nijifiche bondeni hata siku ya tatu jioni.