1 Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria.
2 Basi Daudi akamwuliza BWANA, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila.
3 Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti?
4 Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako.
5 Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng’ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila.
6 Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake.
7 Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo.