18 Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini.
19 Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia.
20 Hata alipokuwa katika kufa, wale wanawake waliohudhuria karibu naye wakamwambia, Usiogope; kwa maana umezaa mtoto mwanamume. Walakini hakujibu, wala hakumtazama.
21 Akamwita mtoto, Ikabodi, akisema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; kwa sababu sanduku la Mungu lilikuwa limetwaliwa, na kwa sababu ya mkwewe na mumewe.
22 Naam, akasema, Huo utukufu umeondoka katika Israeli; maana sanduku la Mungu limetwaliwa.