6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za BWANA; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia BWANA dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa.
7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti.
8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti.
9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia BWANA kwa ajili ya Israeli; BWANA akamwitikia.
10 Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini BWANA akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli.
11 Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari.
12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa BWANA ametusaidia.