16 Akasema, Fuatana nami, ukaone wivu wangu kwa BWANA. Wakampandisha garini mwake.
17 Naye alipofika Samaria, aliwapiga wote waliomsalia Ahabu katika Samaria, hata akamwangamiza, sawasawa na neno la BWANA alilomwambia Eliya.
18 Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.
19 Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; ye yote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali.
20 Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza.
21 Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu ye yote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango.
22 Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.